Katika suala la kucheka na nyavu ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ni ligi namba nne kwa ubora Afrika, Yanga hawana utani wakiwa ni namba moja kwenye eneo hili kwa kukusanya mabao mengi zaidi.

Baada ya mechi 22 ambazo ni dakika 1,980 safu ya ushambuliaji ya Yanga ni namba moja ikiwa imetupia jumla ya mabao 58 ikiwa na wastani wakufunga bao moja kila baada ya dakika 34.
Timu hiyo ilianza kwa mwendo wa kusuasua mzunguko wa kwanza ambapo mchezo wake wa kwanza ikiwa ugenini Agosti 29 2024 dhidi ya Kagera Sugar baada ya dakika 90 ubao ulisoma Kagera Sugar 0-2 Young Africans na mchezo wa pili ilikuwa Ken Gold 0-1 Yanga.
Katika dakika 180 safu ya ushambuliaji ya Yanga ilitupia mabao matatu huku ukuta ukiwa haujaruhusu bao ndani ya mechi hizo za ugenini ambapo bao la ushindi kwenye mchezo dhidi ya Ken Gold, Uwanja wa Sokoine, Mbeya lilifungwa na Ibrahim Bacca ambaye ni beki namba moja kwa kutupia mabao mengi ambayo ni manne.
Ukitazama chati ya utupiaji ndani ya kikosi cha Young Africans kinachonolewa na Miloud Hamdi kuna mastaa wawili ambao kila mmoja katupia mabao 10 kibindoni ndani ya Ligi Kuu Bara.
Prince Dube huyu ni nyota wa kwanza kufunga hat trick na Clement Mzize ni mzawa namba moja mwenye mabao mengi ndani ya ligi namba nne kwa ubora Afrika. Hapa ndipo ambapo upepo ulibadilika baada ya Dube kufungua ukurasa wa mabao ilikuwa ni Desemba 19 2024, Uwanja wa KMC, Complex.



