Kwenye vita ya kuwania ubingwa ndani ya ligi kuu bara inayodhaminiwa na NBC ngoma bado ni mbichi huku Simba ikipigwa bao mazima na Yanga kwenye eneo la kucheka na nyavu.

Kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Miloud Hamdi ni namba moja kwenye timu zenye mabao mengi ambayo ni 58 baada ya mechi 22 ambazo ni dakika 1,980 ikiwa na wastani wakufunga bao moja kila baada ya dakika 34.
Wakati Yanga ikiwa ni namba moja imewapiga bao watani zao wa jadi Simba kwenye eneo hilo kwa kuwaacha kwa tofauti ya mabao sita kwa kuwa safu ya ushambuliaji ya Simba imetupia jumla ya mabao 52.
Kikosi cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids inafuatiwa kimetupia mabao 52 baada ya kucheza mechi 21 ambazo ni dakika 1,890 msimu wa 2024/25 kikiwa na wastani wakutupia bao moja kila baada ya dakika 36.
Mnyama kwa msimu wa 2024/25 imekuwa na wastani wakufunga bao kwenye kila mchezo ambapo katika mechi 21 ambazo ilicheza ni mchezo mmoja pekee ilikwama kufunga ilikuwa dhidi ya Yanga.


