Kilichotokea inawezekana siyo kilichotarajiwa na wengi, baada ya mchezo wa Dabi ya Kariakoo Yanga akiwa mwenyeji uliochezwa jana uwanja wa New Amani Zanzibara kumalizika kwa suluhu na kuacha kelele za mashabiki wa Simba kudhulumiwa goli lao.

Wengi waliipa nafasi kubwa ya Yanga ya kushinda mchezo huo, lakini baada ya filimbi ya mwisho sifa zikienda zaidi kwa Simba kuwa walikuwa na mchezo mzuri zaidi na walistahili kushinda achilia mbali goli la Selemani Mwalimu la dakika za mwisho kukataliwa na Line One.
Huu ulikuwa mchezo wa kwanza Simba wanaitawala Yanga kwa dakika nyingi katika michezo ya hivi karibuni, huku ikiwatumia wachezaji wake wapya, Libase Gueye, Anicet Oura, Inno Liemba ambao waliipa shida kubwa safu ya ulinzi ya Yanga kwa muda wote wa mchezo na Simba kumaliza ikiwa inaongoza kwa mambo mengi, mashuti yaliyolenga lango 4-3, mashuti yaliyotoka nje 5-4, lakini umiliki wa mchezo vipindi vyote walikuwa mbele kwa jumla ya asilimia 54-46 za Yanga.
Kabla ya mchezo huu, Simba ilikuwa imepoteza michezo sita mfululizo ya ligi dhidi ya Yanga lakini mabadiliko makubwa kwenye kikosi yaliyofanywa na kocha wa timu hiyo Steven Barker yamebadilisha mambo mengi kwenye kikosi hicho.
Hata hivyo, kipindi cha pili Simba ilifanikiwa kuuweka mpira kimiani kupitia kwa mshambuliaji wake Seleman Mwalimu lakini mwamuzi wa akiba aliyoosha kibendera, ingawa marudio ya tukio hayakuonyesha tatizo lolote jambo ambalo limezua gumzo mitandaoni.
Pamoja na Simba kutawala kwenye eneo la kushambulia, lakini ni dhahiri kuwa pongezi kubwa zinakwenda kwa kipa wa kimataifa wa timu ya Yanga, Djigui Diarra kutokana na ubora wa juu ambao alifanikiwa kuuonyesha kwa kuokoa michomo kadhaa mikali na mwisho alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo ambao ulikuwa bora na kuvutia.
Katikati mwa kipindi cha kwanza Dickson Job ambaye ni nahodha wa Yanga aliumia na kumpisha Bakari Nondo Mwamnyeto ambaye alifanikiwa kuituliza timu hiyo kwenye eneo la ulinzi huku akiiwahi mipira mingi ya juu na kuwazuia Simba kupata bao.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga iendelee kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 29 zikiwa ni tano mbele ya Simba iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 24.


