Manchester United wamepata pigo kubwa la usajili baada ya nyota wa PSG, Gianluigi Donnarumma, kuripotiwa kukubaliana masharti binafsi na mahasimu wao wa Ligi Kuu ya England, Manchester City.
Awali, United walikuwa na matumaini ya kumnyakua kipa huyo wa Italia kama mrithi wa André Onana, ambaye amekuwa akihusishwa na kurejea Inter Milan, lakini City wameonekana kuwapiga bao la dakika za jioni.

Donnarumma, ambaye ameshindwa kufikia makubaliano ya mkataba mpya na PSG, alionekana akiwa na hisia kali alipowaaga mashabiki wa klabu hiyo mjini Paris siku ya Ijumaa. Jumapili asubuhi, mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, alithibitisha kupitia taarifa yake: “Donnarumma amekubaliana masharti binafsi na Manchester City, na yupo tayari kujiunga na Pep Guardiola. Mazungumzo kati ya City na PSG yanaendelea, na ada inatarajiwa kuwa chini ya euro milioni 50 ambazo awali ziliombwa.”
Hata hivyo, ili dili hilo likamilike, kipa wa Brazil, Ederson, huenda atalazimika kuondoka City, huku akihusishwa na uhamisho kuelekea Galatasaray.
City kwa sasa wanamtumia James Trafford kama kipa wao namba moja, lakini kijana huyo wa England alisahau siku yake dhidi ya Tottenham baada ya kutoa zawadi ya goli katika kichapo cha 2-0 kilichochezwa Etihad siku ya Jumamosi.

Kwa mujibu wa taarifa, Manchester City bado hawajafikia kiwango cha pesa kinachoombwa na PSG, lakini thamani inaweza kushuka kadri dirisha la usajili linavyokaribia kufungwa, kwani klabu ya Ufaransa inahatarisha kumpoteza Donnarumma bure mwakani.
Kwa upande wa Manchester United, kipa huyo wa Italia alikuwa sehemu ya orodha yao ya walengwa wa msimu huu wa joto, wakizingatia kwamba Onana amekuwa na changamoto za kiafya na mustakabali wake umeendelea kuzua gumzo.

