Akiwa na umri wa miaka 27, Eberechi Eze hatimaye anaenda kuishi ndoto ambayo wengi waliitabiri miaka mingi iliyopita, kucheza kwenye moja ya klabu kubwa sita za jadi za Ligi Kuu ya England. Kiungo huyo wa kimataifa wa England anatarajiwa kuondoka kusini mwa London kuelekea kaskazini, lakini si upande ambao wengi walidhani.

Kwa wiki kadhaa, Tottenham Hotspur walionekana kuwa karibu kufanikisha dili na Crystal Palace, huku Eze mwenyewe akionyesha nia ya kuwa nyota mpya katika mpango wa ujenzi wa Thomas Frank. Lakini ghafla, nyota huyo anaelekea kwenye klabu yake ya utotoni, Arsenal, klabu ile ile iliyomwacha akiwa na umri wa miaka 13.
Kwa mashabiki wa Gunners, usajili huu ni sura nyingine kwenye historia ndefu ya uhasama wao na Spurs. Arsenal wamekuwa na tabia ya kuumiza majirani zao mara kwa mara, iwe ni kutwaa ubingwa pale White Hart Lane au kumnyakua Sol Campbell katika moja ya usajili huru maarufu zaidi kwenye historia ya soka la Uingereza. Kumchukua Eze kutoka mikononi mwa Tottenham ni ishara nyingine ya “ushindi” dhidi ya mahasimu wao wa Kaskazini mwa London.
Hata hivyo, uhamisho huu ni zaidi ya historia. Kwa Eze binafsi, ni safari ya kihisia ya kurejea nyumbani, lakini pia changamoto kubwa. Akiwa Palace, ndiye aliyekuwa moyo na ubongo wa kikosi, akibeba jukumu kubwa la ubunifu na mashambulizi. Lakini Arsenal anaingia kwenye kikosi kilichojaa vipaji na kila aina na mfumo ambao tayari umejengwa kuzunguka nyota waliothibitishwa kama Martin Ødegaard, Bukayo Saka na Rice.

Jambo la kuvutia zaidi ni kwamba safari ya Arsenal kumnyatia Eze haikuwa rahisi. Mwanzoni mwa majira ya joto walimfuata kupitia kambi yake lakini wakaonekana kurudi nyuma baada ya chipukizi Ethan Nwaneri kuthibitisha kubaki na klabu. Kwa hatua hiyo, Arsenal walionekana hawana tena haraka ya kusajili kiungo mwingine mbunifu. Kufikia mwishoni mwa Julai, walikuwa tayari wamekamilisha usajili wa wachezaji sita akiwemo Noni Madueke kutoka Chelsea, na walionekana kuridhika.
Lakini fursa ya ghafla ya kumpata Eze na hamu yake ya kurejea Arsenal iliwashawishi hasa walipoona Spurs wakiweka presha kubwa. Kujiamini kwa Tottenham kulitengeneza hali ya maumivu makali zaidi baada ya Arsenal kuingilia dili hilo

Hata hivyo, changamoto kwa Arteta bado ipo. Kikosi chake tayari kimejaa, huku nyota kama Oleksandr Zinchenko, Jakub Kiwior, Albert Sambi Lokonga, Fabio Vieira na Reiss Nelson wakikosa nafasi kwenye mchezo dhidi ya Manchester United licha ya kuwa fit. Kumuweka Eze bila kuvunja uwiano wa kikosi itakuwa kazi nyeti kwa kocha huyo wa Kihispania.

