Usiku wa juna Luis Diaz aliwaka moto kwa kufunga hat-trick ya kuvutia huku Harry Kane akipachika mabao mawili kwa njia ya penalti, Bayern Munich wakiiadhibu Hoffenheim kwa ushindi mnono wa 5-1 katika dimba la Allianz Arena.

Mechi hii ya vigogo wawili wa juu Bundesliga ilianza kwa kasi ya juu. Aleksandar Pavlovic alikaribia kufunga kwa kichwa kilichokwenda nje kidogo ya lango, huku Josip Stanisic akiokoa jahazi kwa upande mwingine kwa kuingilia mchezo wakati muafaka.
Dakika ya 17 ilileta tukio la kustaajabisha. Akpoguma alionekana kumvuta Diaz ndani ya eneo la hatari akimnyima nafasi ya wazi ya kufunga, na mwamuzi pamoja na VAR waliamua penalti na kadi nyekundu. Kane hakufanya kosa, akafunga kwa utulivu na kuipatia Bayern uongozi.
Hata hivyo, Hoffenheim hawakukata tamaa licha ya kuwa pungufu. Ozan Kabak alipata nafasi safi ya kichwa lakini mpira ukagonga mwamba wa juu, kabla ya Kramaric kujaribu shuti lililookolewa na Manuel Neuer.

Dakika ya 35, wageni walisawazisha kufuatia kosa la Neuer. Kipa huyo alijaribu kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma lakini pasi yake ilinaswa na Fisnik Allsani, ambaye alimpa Kramaric mpira wa kufunga kirahisi.
Lakini matumaini ya Hoffenheim hayakudumu. Diaz alilazimisha penalti ya pili baada ya kuchezewa vibaya ndani ya boksi, na Kane tena akapiga kwa nguvu kuirejesha Bayern mbele. Kisha katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza, Kane aliongoza shambulizi la kushtukiza na kumpasia Diaz aliyemalizia kwa ustadi, na kuifanya 3-1 kabla ya mapumziko.
Kipindi cha pili kilithibitisha tofauti ya ubora wa wachezaji kati ya timu hizo mbili. Winga, Michael Olise alitoa pasi safi iliyomkuta Diaz akiwa karibu na lango, naye akufanya makosa, alifunga bao lake la pili.
Mwisho wa mechi, wote Kane na Diaz walikaribia kukamilisha hat-trick, lakini ilikuwa ni Diaz aliyefanikiwa kuondoka na mpira. Alifunga bao la tatu kwa shuti kali, akihitimisha ushindi mkubwa wa Bayern ambao umerejesha morali baada ya kupoteza na kutoa sare katika mechi mbili zilizopita za ligi.


