Baada ya kupoteza mchezo wa hatua ya robo fainali ya kwanza Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry, uongozi wa Simba umebainisha kuwa sababu iliyowafanya washindwe kupata ushindi ni kukwama kutumia nafasi ambazo walizipata kwenye mchezo huo.

Simba chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids, Aprili 2 2025 baada ya dakika 90 walishuhudia ubao wa Uwanja wa Suez Canal ukisoma Al Masry 2-0 Simba ambapo kwenye eneo la ushambuliaji Fadlu alianza na Leonel Ateba.
Mabao kwenye mchezo huo yalifungwa kila moja kipindi chake, ambapo kipindi cha kwanza ni Abderrarhim Deghmoum alianza kupachika bao la uongozi dakika ya 15 kwa shuti kali akiwa nje ya 18 likimshinda Moussa Camara.
Kipindi cha pili ilipachikwa kamba ya pili ambayo ni mali ya John Okoyo dakika ya 89. Mfungaji wa bao la pili alianzia benchi kwenye mchezo huo alipoingia alipachika bao hilo akiwa ndani ya 18.
Murtaza Mangungu, Mwenyekiti wa Simba amebainisha kuwa walikuwa na uwezo wakupata matokeo ugenini jambo ambalo lilishindikana kutokana na nafazi walizotengeneza kushindwa kutumiwa.


