Tottenham Hotspur wako pointi mbili tu juu ya mstari wa kushuka daraja huku zikiwa zimebaki mechi nne kumaliza msimu wa Ligi Kuu ya Uingereza.

Youssouf Fofana amekuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza tangu ajiunge na AC Milan kutoka AS Monaco mwaka 2024.
Tottenham wanazingatia kufanya uhamisho wa majira ya joto kwa nyota huyo wa Milan ili kuimarisha safu yao ya kiungo, kwa mujibu wa jarida la Gazzetta dello Sport. Klabu hiyo ya London Kaskazini inatarajiwa kuimarisha eneo la kiungo baada ya msimu kuisha, huku nafasi ya kiungo mkabaji (namba sita) ikiwa kipaumbele.
Kuna wasiwasi kuhusu mustakabali wa João Palhinha na Yves Bissouma ndani ya Tottenham. Mabingwa wa Europa League 2025 walimsajili Palhinha kwa mkopo wa msimu mmoja kutoka Bayern Munich baada ya kuondoka Fulham, lakini bado kuna mashaka kama watamfanya kuwa mchezaji wa kudumu mwishoni mwa msimu.
Kutokana na hali hiyo, pamoja na sintofahamu ya mustakabali wa Bissouma, Spurs wanafikiria kumsajili Fofana.
AC Milan wanatarajiwa kuhitaji angalau €25m kwa ajili ya Fofana. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 amekuwa muhimu kwa klabu hiyo tangu ajiunge nayo mwaka 2024. Hata hivyo, Rossoneri wanaweza kukubali kumuuza iwapo klabu itatoa dau linalofanana na walilolipa Monaco miaka miwili iliyopita.


