André Onana alihamia kwa mkopo katika klabu ya Trabzonspor mwaka jana, lakini anatarajiwa kurejea katika klabu ya Manchester United mwishoni mwa msimu.

Onana amekuwa akicheza mara kwa mara kwa Trabzonspor msimu huu. Hata hivyo, Manchester United wamearifiwa kuwa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uturuki haiko tayari kulipa kati ya £40 milioni hadi £43 milioni ili kumsajili kipa huyo majira ya kiangazi, kwa mujibu wa ripoti ya MEN.
Onana alijiunga na Trabzonspor kwa mkopo mwezi Septemba baada ya kushuka katika chaguo la makipa ndani ya Manchester United kufuatia ujio wa kipa wa Ubelgiji Senne Lammens.
Lammens sasa amejiimarisha kama kipa namba moja katika uwanja wa Old Trafford baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mechi kadhaa alizocheza kwa klabu hiyo.
Manchester United walitarajia Onana angeonyesha kiwango kizuri akiwa Trabzonspor ili klabu hiyo ya Uturuki iwe tayari kumsajili moja kwa moja, kwani timu hiyo ya Premier League inataka kurejesha sehemu ya ada ya takribani £43.8 milioni waliyoilipa Inter Milan mwaka 2023 kumsajili kipa huyo wa Cameroon.
Ingawa Mlinda Mlango huyo ameanza mechi 20 za ligi kwa Trabzonspor wanaoshika nafasi ya tatu, kipa huyo mwenye umri wa miaka 29 amekuwa akikosa uthabiti wa kiwango akiwa chini ya kocha Fatih Tekke.
Kutokana na hali hiyo, Manchester United wamejulishwa kuwa Trabzonspor hawako tayari kuongeza muda wa golikipa huyo kubaki klabuni hapo baada ya msimu kumalizika.


