Kocha Mkuu wa Yanga Muargentina Miguel Gamondi amezipa tahadhari timu za Ligi Kuu Bara. Hiyo ni baada ya timu yake kuanza vema kwa kushinda mechi mbili mfululizo mabao 5-0 walipocheza dhidi ya KMC na JKT Tanzania.

Yanga pia ilipata ushindi wa mabao 5-1 walipocheza dhidi ya ASAS FC ya nchini Djibouti katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Gamondi alisema kuwa timu pinzani hazitakiwi kujilinda zaidi wanapokutana na badala yake kufunguka kwa kucheza soka kama hawataki kufungwa tano.
Gamondi alisema kuwa timu yake inapata ugumu inaopokutana na wapinzani wanaocheza soka la pasi na kushambulia, hiyo inawafanya wapate ugumu wa kushambulia.

Aliongeza kuwa timu ikijilinda sana, inawapa nafasi ya wao kufanya mashambulizi kwa kasi huku wakianza kuwakabia kuanzia golini kwa wapinzani.
“Wapinzani wenyewe ndio wanataka tuwafunge mabao matano, ni kutokana na kucheza soka la kujilinda kwa kukaa wengi golini kwao. Wao kama hawazitaki tano, basi wasijilinde na badala yake wanapaswa kushambulia kwa kucheza soka la pasi.”
Kwani wakijilinda sisi tunapata nafasi ya kushambulia goli la wapinzani kwa kasi tukiwatumia viungo kupiga pasi za mabao, alisema Gamondi.

