UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa licha ya utani wa jadi uliopo baina yao na Simba bado kuna jambo wanalisikitikia hasa kumuacha kiungo mzoefu, Jonas Mkude.
Mkude Juni 22, ‘Thank You’ kutoka Simba ilipita naye baada ya mkataba wake kuisha hivyo kwa sasa yupo huru akitajwa kuwa kwenye rada za watani zao wa jadi, Yanga.Ikumbukwe kwamba nyota huyo alipandishwa kutoka timu ya vijana ya Simba akiwa ni mchezaji aliyedumu kwa muda wa miaka 13 chini ya Kocha Seleman Matola ambaye kwa sasa anafundisha timu za vijana.
Ally Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga ameweka wazi kuwa, licha ya utani wa jadi dhidi ya Simba lakini watani zao hao walifanya jambo gumu kumuacha kiungo Mkude kiwepesi.
“Unapomzungumzia Mkude (Jonas) yule ni kiungo mzuri na uzoefu kumuacha kirahisi ujue inahitaji kuwe na sababu maalumu lakini haizuii kusema kuwa ni mchezaji mzuri.“Watani zetu wa jadi kwa wanachokifanya sasa acha tusubiri ninadhani msimu ujao watakuwa na kumbukumbu nzuri kwa kuwa watapata majuto na ninachojua mimi Mkude kwenye timu yoyote ile anacheza,” alisema Kamwe.
Legend mwingine ambaye hayupo na Simba ni Erasto Nyoni ambaye huyu ametambulishwa ndani ya kikosi cha Namungo.