Uli Hoeness ni nembo halisi ya FC Bayern Munich, akitumia misimu tisa klabuni hapo kama mchezaji kabla ya kuingia kwenye nafasi za uongozi. Kwa sasa, mwenye umri wa miaka 74 ni mjumbe wa bodi, baada ya pia kuwahi kuwa rais wa klabu na meneja mkuu.
Katika mahojiano ya hivi karibuni na DPA, Hoeness aliweka wazi kabisa msimamo wake iwapo Liverpool watajaribu kumsajili Michael Olise kwenda Merseyside.
“Mkumbuke Liverpool walitumia €500 milioni majira ya joto yaliyopita na bado wana msimu mbaya sana. Hivyo hatutachangia wao kucheza vizuri zaidi msimu ujao.” Alisema.
FC Bayern Munich wanaendelea kufanya vizuri katika Bundesliga na wamefuzu hatua ya robo fainali ya UEFA Champions League, huku Michael Olise akiwa mhimili mkubwa wa mafanikio hayo.
Winga huyo Mfaransa amefunga mabao 11 na kutoa pasi za mabao 18 katika mechi 25 za Bundesliga, pamoja na kuongeza mabao matatu na pasi nne za mabao katika mechi tisa za Champions League.

Bayern walimsajili Olise kutoka Crystal Palace mwaka 2024, na sasa wanamuona kama mmoja wa vipaji bora zaidi duniani. Ana mkataba hadi 2029 na inaripotiwa kuwa hana kipengele cha kuachiliwa (release clause).
Ingawa amekuwa akivutia klabu kubwa kama Real Madrid CF na Liverpool, Bayern wanasisitiza kuwa hauzwi. Mkurugenzi wa michezo wa Bayern, Max Eberl, pia alipuuza kabisa uwezekano wa Olise kuondoka katika mazungumzo na Sport Bild
“Hatuwazii hata kidogo hilo. Yeye ni mchezaji wa Bayern Munich na ana kila fursa hapa ambayo wachezaji wakubwa wanahitaji. Tunataka kujenga mustakabali pamoja naye.”
Afisa mkuu mtendaji wa klabu hiyo, Jan-Christian Dreesen, alisisitiza msimamo huo huo akisema: “Haijalishi ni klabu gani itajaribu kumshawishi: yeyote anayeichezea Bayern Munich anajua thamani ya kuwa hapa.”