Aliyewahi kuwa kocha wa Manchester United, Jose Mourinho ambaye aliweza kupumzishwa na uongozi wa timu hiyo kutokana na mwenendo mbovu na matokeo mabovu ndani ya kikosi hicho; bado amekuwa ni mtu wa maneno mengi na anaongea vile anayojisikia na kuanika hali halisi zote anazopitia kwa sasa tangu awe mtu huru.

Kocha huyo anasema tangu atimuliwe na Manchester United hadi sasa amezikataa ofa tatu za kurudi viwanjani kuongoza timu. Anajiona ni mwenye furaha na aina hiyo ya maisha kwa sababu yanamfanya ajisikie huru na mwenye uwezo wa kufanya lolote analojisikia yeye. Sio hivyo tu pia anafurahia maisha yake kwa sasa kwa sababu kurejea kwake uwanjani kwa wakati huu kunamfanya arudi kwenye mawazo tena kama awali.

Anaendelea kusema kwamba kuwa nje ya kazi hiyo ya kufundisha sio kwamba ameachana nayo, ni kwa nia yake ya kutaka kupumzika kwanza katika hilo na kujaribu kujifunza zaidi na kuangalia mahala ambapo patakuwa sahihi kwake kwa wakati uliopo. Japo kwa sasa hajafikiri kurudi uwanjani kwa siku za usoni.

Kwa sasa kocha huyo anajihusisha na masuala ya michezo bado kiuchambuzi kwenye chaneli ya beIN sports. Kwa sasa anasema anaifurahia kazi hiyo kwa sababu haimpi mawazo wala kikwazo chochote kiutendaji na anaona ni bora aendelee kuitumikia kazi hiyo kwa wakati wote huu uliopo kabla ya kurejea uwanjani.

Kocha huyo amejaribu kugusia sakata lake la kuondoka ndani ya klabu hiyo ya awali kwamba alikosa ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi wake wa juu. Akajaribu kutoa baadhi ya mifano kwamba; hata Pep Guardiola wa Manchester City na Juergen Klopp wa Liverpool walipokea ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi wao.

Anamzungumzia Klopp kwa kusema alipata msaada wa kutosha klabuni hapo kwa kuruhusiwa kusajili wachezaji wengi sana kama: Alisson Becker, Virgil Van Dijk, Andrew Robertson, Mohamed Salah, Roberto Firmino, Sadio Mane, Fabinho, Georginio Wijnaldum, na Naby Keita kitu kinachowafanya wawe vizuri sana.

Pia, akamzungumzia Guardiola kwamba alipewa ushirikiano wa kuuza na kununua wachezaji anaowataka. Aliweza kuwauza mabeki Zabaleta, Sagna, Kolarov na Clichy huku akisajili wapya kama vile Danilo, Walker, Mendy: kitu ambacho yeye hakuweza kukipata.

Hadi sasa anasema hadhani kama atarudi Uingereza lakini amejiandaa na anazidi kujiandaa kama vile alivyofanya akiwa Inter Milan kwa sababu alifanya makubwa sana msimu ule na hali ile ilimjenga na kujiona ni kocha mwenye thamani kubwa katika soka. Na kwa wakati uliopo anajinoa vizuri ili afanye makubwa akipata timu ya chaguo lake.

2 MAONI

JIBU

Tafadhali andika maoni yako
Tafadhali andika jina lako hapa