Saratani ya Pele imeongezeka na nyota huyo wa Brazil atatumia Krismasi akiwa hospitalini kuangalia afya yake.

Mshindi huyo mara tatu wa Kombe la Dunia ametumia wiki tatu zilizopita katika Hospitali ya Israelta Albert Einstein mjini Sao Paulo. Pele amekuwa na saratani ya utumbo mpana tangu 2021 na aliondolewa uvimbe mnamo Septemba mwaka huo.
Amekuwa akitibiwa mara kwa mara na ripoti kutoka hospitalini siku ya Jumatano ilisema kwamba anahitaji huduma ya ziada inayohusiana na matatizo ya figo na moyo.
Pele mwenye umri wa miaka 82 atakuwa hospitalini kwa ajili ya Krismasi, bintiye Kely Nascimento alifichua kwenye mitandao ya kijamii. Katika mtandao wa Instagram, aliandika: “Krismasi yetu nyumbani imesimamishwa.”

“Tuliamua na madaktari kwamba, kwa sababu mbalimbali, ingekuwa bora kwetu kukaa hapa kwa uangalifu wote ambao familia hii mpya huko Einstein inatupa, mapenzi yako kwake, hadithi zake na maombi yake ni faraja kwasababu tunajua hatuko peke yetu.”
Ripoti ya hospitali hiyo ilisema Edson Arantes do Nascimento [Pele] anaonyesha kuendelea kwa ugonjwa huo wa saratani na anahitaji uangalizi mkubwa zaidi kuhusiana na matatizo ya figo na moyo.

“Mgonjwa anasalia hospitalini katika chumba cha kawaida, chini ya uangalizi muhimu wa timu ya matibabu.”

