Kocha wa Real Madrid, Alvaro Arbeloa, alisema uamuzi wa kumtoa nje kwa kadi nyekundu Eduardo Camavinga “uliharibu” robo fainali ya Ligi ya Mabingwa jana baada ya timu yake kutolewa na Bayern Munich.

Real Madrid wamelaani kadi nyekundu “isiyoaminika” baada ya kipigo chao dhidi ya Bayern Munich kilichowafanya waondolewe kwenye ligi ya Mbaingwa.
Kocha wa Real Madrid, Alvaro Arbeloa, alisema uamuzi wa kumtoa nje Eduardo Camavinga “uliharibu” robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ya Jumatano baada ya timu yake kutolewa na Bayern Munich.
Camavinga, aliyeingia kama mchezaji wa akiba, alipata kadi mbili za njano kwa haraka na kutolewa nje zikiwa zimesalia dakika nne katika mchezo wa marudiano wa robo fainali.
Mchezo huo ulikuwa sare wakati Camavinga alipoonyeshwa kadi nyekundu, lakini Bayern walifunga mabao mawili ya dakika za mwisho na kushinda 4-3 usiku huo, 6-4 kwa jumla, na kujipatia nafasi ya kukutana na mabingwa watetezi Paris Saint-Germain katika nusu fainali.

Kadi ya pili ya njano kwa Mfaransa huyo ilionekana kutolewa kwa kuchelewesha kuanza upya kwa mchezo baada ya kumchezea vibaya Harry Kane.
“Ni jambo la kushangaza kwamba unaweza kumtoa mchezaji kwa tukio kama hili katika mechi ya aina hii. Tunahisi huzuni sana, hasira na kukata tamaa. Hii ilionekana kama mchezo wa maamuzi katika msimu wetu.” alisema Alvaro Arbeloa akizungumza na TNT Sports.
Akizungumza na Movistar, Arbeloa alisema mwamuzi “alihujumu” mechi kwa kumtoa Eduardo Camavinga, akidai kuwa huenda hakujua tayari alikuwa na kadi ya njano.
“Nadhani mwamuzi hata hakujua alikuwa na kadi ya njano, ndiyo maana alifanya hivyo, lakini ameiharibu mechi ya mtoano, mchezo ambao ulikuwa mzuri sana, wa kiwango cha juu, na hapo ndipo mchezo ulipoishia.”
Akipita mbele ya waandishi wa habari baada ya mechi, kiungo wa Real Madrid Jude Bellingham alisema uamuzi huo ulikuwa “mzaha”, huku Antonio Rudiger akisema watu walijionea wenyewe hali ilivyokuwa bora wasizungumze.

Kwa upande mwingine, Luis Diaz, aliyefunga muda mfupi baadaye na kuipa Bayern Munich uongozi kwa jumla, aliunga mkono uamuzi wa mwamuzi akisema Camavinga alizuia mashambulizi ya wenyeji kwa kushikilia mpira.
“Nadhani mwamuzi alikuwa sahihi kumtoa. Tulitaka kupiga mpira wa adhabu haraka lakini hakuuachia mpira,” Diaz aliwaambia waandishi.
Kipigo hicho kinaifanya Real Madrid kumaliza msimu wa pili mfululizo bila taji kubwa, huku wakiwa nyuma kwa pointi tisa dhidi ya vinara Barcelona na mechi saba pekee zilizobaki katika La Liga.

