Hapo jana kamati ya Rufaa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imetangaza kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 84 cha Kanuni za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), Timu ya Taifa ya Senegal imepoteza mechi ya fainali ya fainali hizo iliyochezwa Januari 18, 2026 na matokeo ya mechi hiyo kuwa ushindi wa mabao 3–0 kwa Morocco.

Senegal iliifunga Morocco bao 1-0 katika fainali kwenye mechi ambayo iliyogubikwa na sintofahamu pale wachezaji wa Senegal walipokataa kuendelea kucheza baada ya wenyeji Morocco kupewa penalti katika muda wa nyongeza huku mechi ikiwa bado bila mabao.
Baada ya kuchelewa kwa takribani dakika 17, hatimaye wachezaji walirejea uwanjani, lakini penalti ya Brahim Diaz iliokolewa kabla ya Pape Gueye wa Senegal kufunga bao la ushindi katika muda wa ziada.
Hata hivyo, matokeo hayo sasa yamebatilishwa na chombo kinachosimamia soka barani Afrika.
Katika taarifa ya CAF, imesema kuwa Senegal “imetangazwa kupoteza mechi ya fainali kwa adhabu,” huku “matokeo ya mechi yakirekodiwa kuwa 3-0 kwa faida ya Morocco.”

Uamuzi huo unafuatia rufaa iliyowasilishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Morocco (FRMF) kuhusu utekelezaji wa vifungu vya 82 na 84 vya Kanuni za AFCON.
Kamati ya Rufaa ya CAF imetoa majibu na ufafanuzi wa baadhi ya hoja za rufaa hiyo. Rufaa iliyowasilishwa na FRMF imekubalika kisheria na uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya CAF umebatilishwa.
Kamati ya Rufaa ya CAF pia imebaini kuwa mwenendo wa timu ya Senegal unaangukia ndani ya wigo wa vifungu vya 82 na 84 vya Kanuni za AFCON.
Mpaka sasa timu hiyo ya Senegal ambayo inanolewa na kocha mkuu Pape Thiaw hawajatoa tamko lolote kufuatia kauli hiyo ya CAF ya kuwanyang’anya ubingwa, licha ya kuweka picha mtandaoni kule Instagrama na kusindikiza na maneno ya “Forever the First”.


