TAARIFA za kuaminika kutoka ndani ya Simba zinaweka wazi kuwa uongozi huo umemalizana na mshambuliaji wa zamani wa Azam FC Shaban Idd Chilunda akiwa kama mchezaji huru.
Mtoa taarifa huyo aliweka wazi kuwa juzi Jumatatu mchezaji huyo alikutana na viongozi na kumsaini mkataba huo ambao utamfanya kwenda kuwasaidia John Bocco na Jean Baleke kwenye eneo la ushambuliaji.
Chanzo hicho kilisema, baada ya ishu ya jezi kuzinduliwa kumalizika leo huko Moshi watamtangaza mchezaji huyo.
“Amesaini miaka miwili ya kucheza Simba, viongozi wameona ni mtu sahihi kwa sasa kwa kuwa ana kipaji na anaweza kuongeza kitu kwenye eneo la ushambuliaji la timu yetu,” kilisema chanzo hicho.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally ili kuweka mizani sawa alisema: “Ukweli ni kwamba Simba bado haijamaliza kusajili. Kwahiyo taarifa zote za kuwa nani ametua na atatua tutazitoa kwa sasa ni jezi kufika Uhuru Peak.”
Chilunda amezaliwa tarehe 20/07/1998 hadi sasa ana umri wa miaka 24. Ameanza maisha yake ya soka kwenye timu za vijana za Azam Fc kuanzia mwaka 2014 baada ya hapo mwaka 2016 akapandishwa rasmi kwenye timu ya wakubwa na kuanza kuitumikia Azam Fc kwa mafanikio makubwa sana.
Mwaka 2018 alijiunga na timu ya Tenerife ya nchini Hispania ambako alikaa hadi mwaka 2019 kwa mwaka mmoja kisha akajiunga na timu ya CD IZARA ya nchini Hispania hadi mwaka 2020 baadaye akarudi nchini na kujiunga tena Azam Fc.
Mwaka 2021 akajiunga na Timu kutoka Morocco inayoitwa Moghreb Tetouan ambapo alihudumu hadi 2022 kisha akarejea tena Azam Fc na alitemwa msimu uliopita.
Kaze awaaga rasmi Yanga.

