Kipindi cha mafanikio makubwa cha Mohamed Salah akiwa na Liverpool kinaelekea kumalizika kwa namna isiyoridhisha baada ya Paris Saint-Germain kuifunga kirahisi timu ya Arne Slot na kuiondoa kwenye Ligi ya Mabingwa, hali itakayowafanya The Reds kumaliza msimu bila taji lolote.

Arne Slot Aingia Kwenye Presha Kubwa Baada ya Liverpool Kuchapwa na PSG ambapo kwa msimu wa pili mfululizo, Liverpool wameondolewa na PSG.
Ousmane Dembele alifunga mabao mawili huku Liverpool wakitolewa tena na mabingwa hao wa Ufaransa kwenye uwanja wao wenyewe. Msimu uliopita, angalau walitoka kwa heshima baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penalti na timu iliyokuja kushinda Ligi ya Mabingwa.
Hata hivyo, zaidi ya miezi 12 baadaye, tofauti ya kiwango kati ya timu hizi mbili ilikuwa kubwa sana katika michezo miwili, ambapo PSG walishinda 2-0 kwenye uwanja wa Anfield jana na kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-0 bila hata kuhitaji kucheza kwa kiwango chao cha juu kabisa.
Baada ya kushinda EPL katika msimu wake wa kwanza, Liverpool waliingia sokoni kwa kutumia zaidi ya pauni milioni 450 (£450m) ili kuendeleza mafanikio ya klabu hiyo yaliyojengwa wakati wa Jurgen Klopp.

Hata hivyo, msimu ulianza kwa msiba baada ya Diogo Jota kufariki katika ajali ya gari alipokuwa anarudi kwa mazoezi ya maandalizi ya msimu. Ni vigumu kupima kwa kiwango gani athari za kihisia kutokana na kumpoteza mchezaji mwenzao zilivyoathiri timu.
Lakini msimu mbaya uwanjani umeweka nafasi ya Arne Slot hatarini, na tayari umeanza kuleta mabadiliko makubwa kwenye kikosi.
Mohamed Salah ameamua kuondoka mapema kwa mwaka mmoja licha ya kusaini mkataba wa miaka miwili miezi 12 iliyopita. Mmisri huyo, aliyewahi kumkosoa vikali Slot mwezi Desemba baada ya kuwekwa benchi, alianza mechi zote mbili dhidi ya Paris Saint-Germain akiwa benchi.
Andy Robertson pia ametangaza ataondoka mwishoni mwa msimu, jambo linalowaacha Virgil van Dijk, Alisson Becker na Joe Gomez kama wachezaji pekee waliosalia kutoka kikosi cha Liverpool kilichoshinda Ligi ya Mabingwa mwaka 2019.
Kwa kutarajia kipindi kigumu cha mpito baada ya enzi ya Klopp, Liverpool walivunja rekodi yao ya usajili mara mbili msimu uliopita kwa kutumia zaidi ya pauni milioni 100 kumsajili Alexander Isak na Florian Wirtz.

Hugo Ekitike, Jeremie Frimpong na Milos Kerkez pia walijiunga, huku Liverpool wakitumia fedha nyingi kuliko klabu yoyote katika dirisha moja la usajili.
Hata hivyo, ili kufadhili mabadiliko hayo, kulikuwa na wachezaji wengi walioondoka kuliko walioingia. Kuondoka kwa Trent Alexander-Arnold na Luis Diaz kumeacha pengo kubwa, huku kikosi kikiwa kifupi kutokana na majeraha mengi.
Kwa mara ya kwanza, wachezaji wote watano wapya walianza katika mchezo wa marudiano dhidi ya PSG, lakini walidumu pamoja kwa chini ya dakika 30 baada ya Ekitike kupata jeraha la tendon ya Achilles linaloweza kumuweka nje hadi msimu ujao.
“Ni sehemu ya msimu wetu. Tulikuwa na Alex, Hugo na Florian pamoja kwa dakika 88 tu kabla ya leo. Tumeongeza dakika 28, na nashangaa kama tutaweza kuongeza zaidi (msimu huu).” Alisema Slot.
Isak, aliyesajiliwa kwa rekodi ya pauni milioni 125 kutoka Newcastle United, alikuwa anaanza kwa mara ya kwanza tangu apate mguu kuvunjika mwezi Desemba.
Msimu wa kwanza wa Frimpong pia umeathiriwa na majeraha ya misuli ya mara kwa mara na alibadilishwa tena mapumzikoni na Gomez. Wirtz amebaki fiti lakini hajaonyesha kiwango kilichomfanya awe nyota wakati akiisaidia Bayer Leverkusen kushinda Bundesliga miaka miwili iliyopita.


