Hansi Flick amewapa changamoto wachezaji wake wa Barcelona kushinda taji la LaLiga “haraka iwezekanavyo” kufuatia kuondolewa kwao katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Barcelona waliibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Atletico Madrid katika mchezo wa marudiano wa robo fainali uliochezwa jana usiku, lakini haukutosha kuwapeleka hatua ya nusu fainali, huku kikosi cha Diego Simeone kikishinda kwa jumla ya mabao 3-2.
Flick alisema kwamba “anajivunia timu” kutokana na kiwango chao cha uchezaji, akichukua mambo chanya kutoka kwenye kuondolewa huko.
Barcelona sasa wameelekeza nguvu zao zote kwenye ligi ya Hispania, ambapo kwa sasa wanaongoza LaLiga kwa pointi tisa mbele ya Real Madrid waliopo nafasi ya pili, huku zikiwa zimebaki mechi saba. Flick amewataka wachezaji wake kumaliza ubingwa “haraka iwezekanavyo.”
Hansi Flick alisema: “Ninajivunia timu na jinsi tulivyocheza. Katika mechi zote mbili nadhani tulistahili nafasi ya kucheza nusu fainali,” Flick aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano wa waandishi baada ya mchezo wa jana”

Flick amesema kuwa walikuwa bora sana katika kipindi cha kwanza, lakini walipaswa kufunga mabao zaidi. Walicheza walicheza vizuri sana na walilazimika kucheza wakiwa na wachezaji 10.
Licha ya kuondolewa, wanapaswa kuendelea kucheza hivi. Kuna watu wengi wameumia na hilo ni kawaida. Kushinda Ligi ya Mabingwa ni muhimu sana na nadhani tuko njiani kuelekea hilo. Kuna nafasi ya kuboresha na hilo ndilo wanalopaswa kufanya.
Kocha huyo anaendelea kusema kuwa anathamini kile alichonacho, ni wazi hawakuwa na bahati nyingi, lakini ndivyo ilivyo na wanapaswa kukubali. Wana timu changa na watazidi kuboreka. Ni vizuri kuzungumzia walichofanya na wanapaswa kujivunia hilo.
“Tumeumia lakini tutarudi tena. Hatua inayofuata ni kushinda ligi. Tunataka kuishinda na haijalishi lini, lakini tunataka kuishinda haraka iwezekanavyo.”

Barcelona tayari wataelekeza macho yao kwenye mechi yao inayofuata ya La Liga, ambayo ni ya nyumbani dhidi ya Celta Vigo tarehe 22 Aprili, kabla ya kumaliza mwezi kwa mchezo wa ugenini dhidi ya Getafe.
Baada ya hapo, kikosi hicho cha Catalonia kitakutana na Osasuna, Real Madrid, Alaves, Real Betis na Valencia katika mechi zao tano za mwisho za ligi mwezi Mei.