Baadhi ya wachezaji mikataba yao ya kuendelea kutumikia klabu husika inaelekea ukingoni kukiwa na walakini wa baadhi yao kuongezewa mikataba hiyo ili kuendelea kuhudumu katika klabu hizo zaidi. Baadhi yao hawana mahusiano na klabu zao kwa sasa na wengine wanaonekana kupewa nafasi ya kuendelea kusalia.
Diego Godin
Amecheza katika klabu ya Atletico kwa muda wa kutosha hadi sasa, amekuwa aina ya walinzi ambao sio rahisi kupitika wakiwa katika majukumu yao uwanjani. Ameanza maisha yake na klabu hiyo tangu ikiwa haina jina kubwa hadi sasa imekuwa mpinzani mkubwa kwa klabu zote kubwa barani Ulaya. Aliweza kuchukua ubingwa mwaka 2014 akiwa na klabu hiyo. Hivi karibuni amekuwa akihusishwa na kujiunga na Inter pia Juventus.
Vincent Kompany
Hakuna wasiwasi mkubwa juu ya maisha yake ya soka kutokana na mchango wake kuonekana wazi ndani na nje ya klabu ya City na kuna uwezekano mkubwa wa kuongezewa kandarasi mpya ya kuendelea kusalia na wababe hao wa soka nchini Uingereza. Kwa kiasi kikubwa amekuwa nguzo katika klabu hiyo kwa kipindi kirefu sana na ana kila sababu ya kusalia hapo.
Antonio Valencia
Yupo tayari kuondoka wakati wowote Manchester United kutokana na kukosa wakati mwingi wa kucheza. Hilo linachangiwa na kukumbwa na majeruhi ya muda mwingi ambayo yamemfanya Ole Gunnar Solskjaer kumwacha katika kikosi mara mwa mara. Hata hivyo, yeye mwenyewe anaona kwa umri wake na makubwa aliyoyafanya na kikosi hicho ana kila sababu ya kucheza soka ambalo litakuwa halina ushindani sana kwake.
James Milner
Akiwa na umri ambao katika hali ya kawaida hali yake ya uchezaji lazima ianze kuwa chini, mchezaji huyo ana asilimia kubwa za kuongezewa mkataba ili aendelee kudumu na kikosi hicho. Amekuwa nguzo kubwa kikosini hapo na ana kila sababu ya kupewa muda mwingine ili akifikishe kikosi hicho kunakotakiwa kwa wakati uliopo.
Adrien Rabiot
Mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 23 amekuwa katika wakati mgumu ili kuweza kukidhi uhitaji wa mwalimu wake. Ni katika kipindi kifupi alionekana kutaka kujiunga na Barcelona ila ndoto hiyo ilipotea ghafla baada ya miamba hao kumsajili De Jong. Na haonekani kama atasalia klabuni hapo kwa wakati uliopo; anahusishwa kunyemelewa na Liverpool na Tottenham.
Gabriel
Habar njema sana 👍