Kocha mkuu wa Chelsea Graham Potter ametoa wito wa kuwa na subira huku akionya kuwa haitakuwa rahisi kupata timu yenye sura mpya ya Chelsea baada ya kutoka sare tasa na Fulham katika mchezo wa jana.

Enzo Fernandez alianza jana kwenye mchezo wake wa kwanza akiwa na jezi ya bluu katika uwanja wa Stamford Bridge siku tatu baada ya kuweka rekodi ya Ligi Kuu ya Uingereza kwa kusajiliwa pauni milioni 106.8 (€121m) kutoka Benfica, huku nafasi ya Mykhaylo Mudryk ikichukuliwa na mchezaji mwenzake Noni Madueke wakati wa mapumziko.
Licha ya kufanya majaribio kadhaa kwenye lango la mpinzani lakini hakuna timu ambayo iliingia kambani na kupachika bao na hatimaye mechi kuisha kwa bila bila.
Chelsea inaeleweka hawajakaa vizuri kwani kuna maingizo mapya ya wachezaji na kocha mkuu Potter anasema watahitaji muda kujenga maelewano.

Potter amesema; “Kulikuwa na msisimko na hali nzuri tangu mwanzo, hali nzuri. Roho ya wachezaji ilikuwa nzuri sana. Walijitahidi kwa kila mmoja dhidi ya timu pinzani na wamekuwa pamoja kwa muda mrefu”.
Kocha huyo wa Uingereza anasema kuwa wanahitaji muda wa kusuluhisha kila kitu. Walikuwa wanakosa uhusiano, uwazi na kujiamini kunatokana na kujuana kila mmoja wao.
“Wakati mwingine lazima uangalie kifurushi kizima. Wachezaji wachanga, mchanganyiko mzuri wao wote wawili. Kwetu, ni kuhusu kuboresha”. Alisema kocha huyo.

Wachezaji wapya wanazoea nchi mpya na ligi mpya. Sio moja kwa moja. Wakati bei ni kama ilivyo, maswali yataulizwa, ni asili ya biashara.
Kurejea kwa Reece James na Ben Chilwell kutoka kwenye majeruhi ilikuwa faida kubwa kwa Chelsea, huku Potter akifichua kuwa winga Mudryk aliondolewa baada ya kusumbuliwa na baridi wiki hii.

