Rais wa Bayern Munich Herbert Hainer amekasirishwa na kitendo chamlinda mlango wao Manuel Neuer kutangaza hadharani ukosoaji wake kwa mabingwa hao wa Bundesliga kwa kumfukuza Toni Tapalovic.

Neuer alielezea uamuzi wa mabingwa hao wa Bundesliga kumuondoa mkufunzi wa makipa Tapalovic kama jambo la kikatili zaidi ambalo amewahi kukumbana nalo katika maisha yake ya soka.
Nahodha huyo wa Bayern aliongeza kuwa kuondoka kwa mshauri wake alipokuwa akipata nafuu kutokana na kuvunjika mguu alioupata wakati wa kuteleza kwenye theluji mwezi Desemba ilikuwa pigo kwake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bayern Oliver Kahn na mkurugenzi wa michezo Hasan Salihamidzic wameweka wazi kuwa hawakufurahishwa na matamshi ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani.

Hainer pia alimkosoa Neuer aliyehudumu kwa muda mrefu siku ya jana akisema kuwa ni jambo lisiloeleweka na la kukatisha tamaa kwao kwamba Manuel hakutafuta njia kwao, lakini alienda moja kwa moja kwa umma.
“Nimesikitishwa zaidi kuliko hasira, kwa sababu ningefikiria kwamba Manuel ambaye amekuwa nasi kwa muda mrefu ana imani kubwa na anakuja kwetu kwanza kujadili. Naunga mkono asilimia mia moja kile Oliver Kahn na Hasan Salihamidzic walisema.”

Hainer alikataa kukatisha mkataba wa Neuer, lakini kuna mashaka iwapo atabaki na unahodha, na sasa amesema kuwa watakaa naye na kushughulikia kila kitu kwa utulivu na weledi.
Jambo muhimu zaidi kwa sasa ni kwamba Manuel atapona tena na anaweza kucheza. Na kisha ndipo wataona.

