SIYO Yanga Princess pekee ambao mpaka sasa wanaozea kambini licha ya kuelekea mwezi wa pili sasa tangu ligi yao ilipomalizika, bali hata The Tigers Queens wapo Arusha na hawajui lini wataondoka.
The Tigers Queens ambao hawatakuwepo kwenye ligi kwa msimu ujao baada ya kushukda daraja, asilimilia 70 ya wachezaji wazawa bado wanasubiri kupewa stahiki zao ili waweze kurudi makwao.
Mmoja ya wachezaji wa klabu hiyo ambaye aliomba hifadhi ya jina alisema, hata kula kwao kumekuwa kwa shida na jambo la kawaida wao kulala njaa na kila wakifanya jitihada za kuzungumza na mmiliki amekuwa akiwaambia kuwa hana fedha.
“Bado tupo kambini hadi leo, wachezaji tunasubiri nauli tu angalau ili turudi makwetu na hatuna hela kusema kweli ya nauli, kula kwetu kwenyewe kumekwa kwa shida pia,” alisema.
Alipotafutwa mmiliki wa timu hiyo Potini Pello Kivuyo ili kujua wapi anakwama, namba yake ilikuwa inaita bila kupokelewa kwa muda mwingi na hata meseji zikawa hazijibiwi.

