LIGI Kuu Wanawake Bara inatarajia kuendelea tena kesho kwa mechi mbili kuchezwa kwenye viwanja viwili. Yanga Princess watakuwa Jamhuri Dodoma kucheza na Baobab Queens.
Huku Ceasia Queens wakitarajiwa kucheza na The Tigers Queens, mchezo ambao unatarajiwa kuchezwa kwenye uwanja wa Mkwawa Iringa.
Yanga imesafiri ikiwa haina ripoti ya wachezaji majeruhi hasa wale tegemeo, huku Baobab Queens nao wakielezwa kuwa wapo kamili kwa mchezo huo.
Mchezo wa mwisho baina ya Baobab Queens na Yanga msimu uliopita kwenye uwanja huo, Yanga Princess walishinda kwa mabao 2-0.
Yanga wamekusanya alama saba kwenye mechi nne walizocheza, wakati Baobab wao wakiwa wamevuna pointi 4 wakiwa nafasi ya 6. Huku Yanga wakiwa nafasi ya 3.
Mchezo wa Ceasia Queens na The Tigers Queens una hatihati ya kutochezwa kesho kwa kuwa mpaka kufikia mchana wa leo Tigers walikuwa hawajasafiri.
Na kama ikiwa hivyo hii itakuwa ni mara ya pili wanafanya hivyo baada ya kushindwa kwenda Dodoma kucheza na Baobab Queens.