Klabu ya Simba wekundu wa Msimbazi wamefanikiwa kuanza ligi kibabe baada ya kupata ushindi wa mabao manne kwa mawili dhidi ya klabu ya Mtibwa Sugar.
Simba walifanikiwa kupata mabao ya mapema kipindi cha kwanza kupitia kwa wachezaji Jean Baleke pamoja na Willy Onana, Lakini wenyeji wa mchezo klabu ya Mtibwa Sugar hawakua wanyonge ambapo walifanikiwa kurudisha mabao hayo mawili kupitia kwa mshambuliaji wa zamani wa KMC Matheo Anthony.
Klabu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu huku Mtibwa Sugar wao wakionekana kufanya mashambulizi ya kushtukiza zaidi, Mpaka pale dakika ya 45 ya mchezo ambapo kiungo Fabrice Ngoma aliipa Wekundu wa msimbazi uongozi kwa kufunga bao la tatu na mchezo kwenda mapumziko.
Mchezo huo ulienda mapumziko Mnyama akiwa anaongoza kwa mabao matatu kwa mawili dhidi ya Mtibwa Sugar, Wakati huo Mnyama akiwa anaonekana anaumiliki mpira zaidi licha ya kua mgeni katika mchezo huo uliopigwa katika dimba la Manungu mkoani Morogoro.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo wekundu wa msimbazi walionekana bado wana njaa ya kutafuta mabao zaidi kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara waliyokua wanayafanya langoni kwa Mtibwa, Ambapo dakika ya 81 mashambulizi yalizaa matunda ambapo Clatous Chama aliipatia Simba bao la nne na la mwisho katika mchezo huo.

