Mgombea urais wa Barcelona, Victor Font, ametoa onyo kali kwa Mkurugenzi wa Michezo wa klabu hiyo, Deco, akisema kuwa atamwondoa kwenye nafasi yake endapo atashinda uchaguzi ujao na kumng’oa Joan Laporta madarakani.
Font ameweka wazi kuwa hana mpango wa kuendelea kufanya kazi na Deco, ingawa ameonesha nia ya kumbakiza kocha wa kikosi cha kwanza, Hansi Flick, endapo atapewa dhamana ya kuiongoza klabu hiyo.
Barcelona kwa sasa inajiandaa na uchaguzi wa urais utakaofanyika mwezi ujao. Laporta anawania tena nafasi hiyo, huku Font, Marc Ciria, Xavier Vilajoana na Joan Camprubi nao wakithibitisha kuwania. Laporta alichaguliwa kwa mara ya pili mwaka 2021 baada ya kupata asilimia 54 ya kura, akiwashinda Font na Toni Freixa.
Akizungumza na RAC1, Laporta alisema anaamini anastahili kuendelea kuiongoza klabu hiyo, akisisitiza kuwa mwaka huu umekuwa wa kurejesha hadhi ya Barcelona. Alidai kuwa uongozi wake umekabiliana na changamoto kubwa, ikiwemo kampeni za kuidhoofisha taasisi pamoja na vikwazo vya usajili wa wachezaji.




