Unaweza kuwa haukuwa usiku mzuri kwa United ambao waliambulia patupu mbele ya Arsenal walioonekana kuwa katika hali ya ubora katika mechi iliyowakutanisha miamba hao wa soka. Kilichovutia sana katika mechi hiyo ni uimara na ubora uliokuwa umetawala timu hizo jambo ambalo lilifanya mechi hiyo kuwa na mvuto wa pekee sana.
Arsenal wanarudi hadi nafasi ya nne sasa kwenye ligi hiyo baada ya kupata ushindi wa 2-0 dhidi ya United. Katika uhalisia wake kwa kipindi cha kwanza walistahili kabisa kuupata ushindi huo mbele ya mpinzani wao. Mara nyingi Arsenal amekuwa akipoteza mechi zake mbele ya United kitu ambacho hata namna United alivyocheza alionekana kuishusha sana mechi hiyo.
De Gea alianza kipindi cha kwanza kwa kufungwa goli ambalo katika hali ya kawaida lilonekana rahisi sana kwake japo ni vitu ambavyo hutokea sana katika soka. Alipotezwa na Xhaka ambaye aliupiga mpira ulioonekana kuelekea upande wake wa kulia lakini ghafla ulibadilishwa uelekeo na kufungiwa upande wa kushoto.
United walijaribu kupigana katika kipindi cha pili ili kurudisha goli hilo mapema iwezekanavyo ndani ya mchezo huo japo juhudi zao zilionekana kugonga mwamba kipindi chote kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Arsenal ambayo haikujaribu kabisa kuwaruhusu United kuingia na mipira kwenye lango lao.
Umekuwa sio msimu mzuri kwa Emery akiwa na kikosi hicho ndani ya msimu huu kutokana na matokeo yake mabovu mbele ya Rennes walipokutana kwenye michuano ya Europa mechi iliyomfanya aambulie kichapo kikali kutoka kwa timu hiyo na kuanza kufifisha matumaini ya kusonga mbele kunako michuano hiyo mikubwa kabisa.
Nafasi yao ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo ya Europa ili kuweza kujiwekea nafasi ya kucheza klabu bingwa mwakani kupitia upande huo imekuwa ngumu sana kutokana na matokeo hayo. Hivyo, tumaini lao kubwa kwa sasa ni kuendelea kupigania nafasi ya nne ndani ya ligi hiyo kusudi waweze kupata upenyo wa kuwa ndani ya michuano hiyo msimu ujao.

Leno alisimama imara katika milingoti yake mitatu kwa kuokoa mipira yote ya hatari iliyopelekwa langoni hapo. Amekuwa mchezaji nyota katika mchezo huo kitu ambacho amestahili kabisa kukifikia kwani mchango wake kuwazuia Rashford na Lukaku wasifunge kila wakiwa na mpira ni cha ushujaa wa hali ya juu.
Macho yote kwa Arsenal sasa hivi ni kumaliza mechi yao dhidi ya Rennes na kuhakikisha wanapata ushindi wa nyumbani ili kufufua matumaini yao ya kuendelea kushiriki ligi hiyo. Mbali na hilo, majirani zao wanajipanda sasa kucheza na Wolves katika mechi yao ya kombe la FA huku wakiwa bado na moto uleule wa kutaka matokeo mazuri ili angalau wapate kikombe cha kuwawezesha kumaliza na chochote msimu huu unaoelekea mwishoni sasa.

