Antonio Conte anapoahirisha mazungumzo ya kuongeza mkataba wake, huwa anafanya hivyo kwa sababu ameamua kuondoka. Ilitokea Juventus, ikatokea Inter Milan na sasa inafanyika Tottenham Hotspur.
Dalili za kutengana na Spurs zote zipo na Conte ana historia nyingi za hivi karibuni za kuihama klabu yake mapema.
Siku chache tu baada ya kusisitiza kuwa mkataba wake ‘si suala la kipaumbele’, Tottenham ilipata kichapo kibaya ambacho kiliwakatisha tamaa mashabiki, kipigo cha 2-0 dhidi ya Manchester United Jumatano.

Wanahabari walipomuuliza kuhusu mkataba wake, kocha huyo wa Italia huwa anapaza sauti na kujibu kwa hisia kwa sababu hapendi maswali ambayo hawezi kuyajibu mara moja.
Anafikiria tu mambo ya uwanjani, mafunzo na matokeo na hataki kusikia juu ya kitu kingine chochote.
Conte ni mtaalamu na atatoa damu, jasho na machozi kwa Tottenham, klabu na mashabiki, hata kama ataamua kuondoka mwishoni mwa msimu. Atatoa asilimia 100 ya nguvu zake kusaidia upande wake wa sasa.

Kwa bahati mbaya, hata hivyo, mkataba wake huko White Hart Lane unamalizika msimu ujao wa joto na ni wakati mwafaka wa kuhamia kwingine.
Conte anahisi anahitaji kuwa katika klabu kubwa na kama hawezi kuipata London, angependelea kwenda nyumbani kwenye familia yake nchini Italia.

