BAADA ya Simba kufanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga huko Tanga kwenye mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Kighoma Malima ameuomba uongozi wa Mtibwa Sugar kuhamishia mechi yao ya kesho kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Awali mchezo kati ya Mtibwa na Simba ulipangwa kupigwa katika Uwanja wa Manungu Complex Turiani, jambo ambalo uongozi huo umebadili na sasa mchezo huo utapigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Mrogoro.Akizungumza mbele ya Wanahabari, Malima alisema wamelazimika kuomba mchezo huo mkubwa na muhimu kupigwa katika Uwanja wa Jamhuri ili kutoa fursa kubwa kwa mashabiki wa mkoani hapo kuingia na kutazama mechi hiyo.
“Tumelazimika kuomba mchezo wetu dhidi ya Simba uhamishiwe kwenye Uwanja wa Jamhuri ili tuweze kutoa fursa kubwa ya mashabiki na wananchi wa mkoa huu kuishuhudia klabu yao pekee kwa wingi, kwani michezo mikubwa kama hii ikipigwa Manungu inatoa fursa ya mashabiki wachache kuingia kutokana na ufinyu wa uwanja huo.“Ili tuweze kuichukulia Mtibwa kama timu yetu ya mkoa ni vyema tukaanza sasa kucheza uwanja wa Jamhuri, na michezo mingine ibaki tu Turiani na Gairo kutokana na uwezo wa timu wanayokutana nayo, kwani kwa kufanya hivi tutaweza kueneza mapenzi makubwa kwa mashabiki wote wa hapa Morogoro,” alisema.