Klabu ya Arsenal imekubali kupokea kichapo cha mabao mawili kwa bila mbele ya klabu ya Aston Villa katika mchezo wa ligi kuu ya Uingereza uliopigwa leo katika dimba la Emirates.
Arsenal wamekubali kupokea kipigo wakiwa nyumbani kwao na kipigo cha pili kutoka kwa klabu ya Aston Villa, Kwani klabu hiyo ilikubali kichapo cha bao moja kwa bila katika mzunguko wa kwanza katika dimba la Villa Park.Washika mitutu hao wa London kama ilivyo kawaida yao walionekana kuanza mchezo kwa kasi na kutengeneza nafasi mara kwa mara, Lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Aston Villa na golikipa wao Emiliano Martinez uliwazuia kupata goli.
Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika klabu hiyo ilikua imemiliki mchezo kwa kiwango kikubwa, Lakini pia kutengeneza nafasi kadhaa ila uimara wa Villa kwenye kuzuia ulifanya mchezo huo kwenda mapumziko kwa sare ya bila kufungana.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na vijana wa Mikel Arteta wakiendelea kulisakama lango la Aston Villa, Lakini Villa waliendelea kua na nidhamu ya uzuiaji na kufanya mashambulizi ya kushtukiza ambapo dakika 84 ya mchezo waliwashangaza Arsenal baada ya Leon Bailey kufunga bao la kwanza dakika ya 87 Ollie Watkins akapigilia msumari wa moto.Kwa matokeo haya washika mitutu wanaendelea kubaki nafasi ya pili na alama zao 71 wakilingana na Liverpool ila wao wako juu kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa, Manchester City wao wanaendelea kuongoza msimamo wa ligi kuu ya Uingereza wakiwa na alama zao 73.