Aston Villa wamekubali dili la kumsaini mchezaji wa kimataifa wa Ubelgiji Youri Tielemans mkataba wake na Leicester iliyoshuka daraja utakapomalizika.

Villa wamethibitisha kuwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26 atajiunga nao Julai 1 baada ya miaka minne katika uwanja wa King Power.
Taarifa kwenye tovuti rasmi ya klabu ilisema: “Aston Villa ina furaha kutangaza kwamba klabu imefikia makubaliano ya kumsajili Youri Tielemans. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji atakuwa Villan rasmi Julai 1 baada ya mkataba wake na Leicester City kumalizika.”
Tielemans alijiunga na Leicester kutoka Monaco kwa mkataba wa pauni milioni 40 mnamo Julai 2019 baada ya kufanikiwa kwa mkopo katika kipindi cha pili cha msimu uliopita, baada ya kuanza kazi yake na Anderlecht.

Kwa jumla, aliichezea Foxes mechi 195 na kufunga mabao 28, likiwemo bao la ushindi walipoichapa Chelsea 1-0 kwenye fainali ya Kombe la FA 2021. Pia aliwakilisha nchi yake kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2018 na 2022 na Euro 2020.

