Arsenal wamefuzu fainali ya Carabao kwa mara ya kwanza baada ya miaka nane, baada ya Kai Havertz kufunga bao la ushindi wa 1-0 dhidi ya Chelsea katika mechi ya marudiano ya nusu fainali jana.

Kikosi cha Mikel Arteta kilikuwa tayari kimejiweka kwenye nafasi nzuri baada ya mkondo wa kwanza, na Havertz aliingia kutoka benchi na kukamilisha ushindi wa jumla wa mabao 4-2 katika dakika za mwisho kwenye Uwanja wa Emirates. Ilikuwa ushindi wa faraja kubwa kwa The Gunners, waliokuwa wamepoteza nusu fainali zao nne zilizopita katika Ligi ya Mabingwa 2025, Kombe la Ligi 2022, Kombe la Ligi 2021 na Europa League 2021.
Katika fainali yao ya kwanza baada ya miaka sita, Arsenal watakutana na Manchester City au Newcastle katika Uwanja wa Wembley Machi 22. City wanaongoza Newcastle kwa mabao 2-0 kabla ya mkondo wa pili utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Etihad.
Arsenal hawajashinda Kombe la Ligi tangu mwaka 1993, na walipoteza fainali zao tatu za mwisho walizocheza. Sasa wana nafasi ya kumaliza ukame huo kwa kutwaa taji lao la kwanza tangu waliposhinda Kombe la FA mwaka 2020. Hilo ndilo taji pekee ambalo Arteta ameshinda tangu alipoteuliwa Desemba 2019.
“Tulijua ingekuwa vita kali uwanjani. Uvumilivu na uelewa wa aina ya mchezo tuliopaswa kucheza vilitusaidia sana. Kulikuwa na hali ya kipekee kabisa uwanjani. Inaleta tofauti kubwa. Tumekuwa tukisubiri kwa miaka kadhaa kufikia hatua hii na kwa hakika tutaifurahia.” Alisema Arteta.

Msimu huu unaonekana kuwa wa kukumbukwa kwa Arsenal, ambao wanaongoza Ligi Kuu ya Uingereza kwa tofauti ya pointi sita na pia wamefuzu hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa baada ya kushinda mechi zote nane za hatua ya makundi.
Licha ya mafanikio yao, Arsenal wamekuwa wakikosolewa kwa kutegemea sana mabao yanayotokana na mipira ya kona na mipira iliyokufa. Arteta alitetea kwa nguvu mtindo wa timu yake wiki hii, akisema ana “orodha kubwa ya watu” wanaoamini kikosi chake ndicho “chenye kuvutia zaidi barani Ulaya.”
Mchezo wa Jumanne ulikuwa mgumu na wa kupambana, lakini Arteta hatajali wakosoaji baada ya kuipeleka timu yake Wembley.
Kocha wa Chelsea, Liam Rosenior, alikuwa ameshinda mechi sita kati ya saba katika mashindano yote tangu alipowasili kutoka Strasbourg kuchukua nafasi ya Enzo Maresca. Hata hivyo, alishindwa kupata suluhisho dhidi ya Arsenal, ambao walimpa vipigo viwili pekee katika kipindi chake kifupi.
“Arsenal walijua walikuwa kwenye mchezo mgumu katika mikondo yote miwili. Tulitawala maeneo tuliyotaka kipindi cha pili, lakini hatukupata ile nafasi ya ubora. Ni uchungu kupoteza. Tunapaswa kuendelea kuboresha, jambo ninaloliona kutoka mkondo wa kwanza hadi wa pili”. Alisema Rosenior.


