Mshambuliaji wa Arsenal Gabriel Jesus anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa takriban miezi mitatu, kulingana na ripoti.

Jesus aliondolewa kwenye mechi zilizosalia za Kombe la Dunia Jumamosi baada ya kupata jeraha la goti akiwa kwenye dimba na Brazil, na suala hilo sasa linaaminika kuwa mbaya zaidi kuliko ilivyohofiwa mwanzoni.
Kulingana na Sport TV kupitia SB Nation, vinara wa Ligi ya Uingereza Arsenal wanaweza kumkosa nyota wao huyo hadi angalau Machi, na hivyo kuathiri sana matumaini yao ya ubingwa.
Jesus alianza katika mechi ya Brazil waliyopoteza kwa bao 1-0 na Cameroon siku ya Ijumaa, lakini alitolewa kipindi cha pili baada ya kuhangaika kupata matokeo kwenye mchezo huo.
Ilikuwa ni mechi yake ya kwanza kuanza kwenye michuano hiyo baada ya mechi mbili akitokea benchi katika ushindi dhidi ya Serbia na Uswizi.

Amekuwa muhimu kwa kiwango kizuri cha Arsenal msimu huu na amekuwa akisifiwa sana na meneja Mikel Arteta mara kadhaa, lakini Mhispania huyo sasa atalazimika kushughulika bila mchezaji huyo wa miaka 25 kwa muda.
Kuna uwezekano Arsenal wataingia sokoni kujiimarisha Januari, huku Eddie Nketiah pekee akiwa na sifa ya namba 9 asilia.
Jesus amefunga mabao matano katika mechi 20 tangu ajiunge na The Gunners majira ya joto kwa pauni milioni 45 akitokea Manchester City.

