Dirisha la uhamisho hufunguliwa kuruhusu uhamisho wa wachezaji kutoka klabu moja kwenda klabu nyingine, au kuruhusu sajili mbalimbali za wanasoka katika klabu. Lakini, tetesi za nani anaenda wapi, au staa gani anatarajia kwenda wapi na klabu ipi inataka kumuuza au kumnunua nani huwa haziishi sambamba na dirisha la usajili! Fununu zinaripoti kuwa Juventus wamempania Paul Pogba!
Juventus walishawahi kumsajili Pogba akiwa kama mchezaji huru akitokea United, kisha wakamuuza tena nyota huyo kwa Manchester United kwa dau la kuvunja rekodi, sasa wanataka wamrejeshe nyota huyu!
Kwa mujibu wa chanzo cha iBiancoNero, Paul Pogba bado yupo kwenye rada ya juventus ambao wanahitaji kumrudisha nyota huyo klabuni kwao. Pogba alitarajiwa angesepa United katika dirisha la usajili la mwezi Januari akihusishwa zaidi na kurejea Juventus baada ya kutokuwa na mahusiano mazuri na aliyekuwa meneja wa klabu hiyo, lakini kufika kwa Ole Gunner klabuni hapo kumerejesha matumaini ya nyota huyu kuendelea kusalia kwa kipindi fulani.
Hata hivyo, wakati Juventus wakidaiwa kuwa wanahitaji kuwaweka paamoja Aaron Ramsey na Paul Pogba, taarifa zinaripoti kuwa mfaransa huyu anaweza kusalia United ikiwa tu watafanikiwa kuingia Ligi ya Mabingwa. Juventus wanadaiwa kuwa na Tanguy Ndombele kwenye rada yao ikiwa watamkosa Pogba.

