Barcelona wamethibitisha kuwa Robert Lewandowski atakuwa sehemu ya kikosi kitakachosafiri kwa ajili ya mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Inter Milan kwenye uwanja wa San Siro usiku wa kesho, huku kocha Hansi Flick akitangaza kikosi chake cha wachezaji 23 watakaosafiri.

Inter Milan na Barcelona kwa sasa wako sare ya mabao 3-3 baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa Montjuïc Jumatano, ambapo mabao yalifungwa na Marcus Thuram, Denzel Dumfries, Lamine Yamal, Ferran Torres na goli la kujifunga la Yann Sommer katika pambano kali lililojaa mabao sita.
Timu hizi mbili zitakutana tena San Siro kuwania nafasi ya kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo mshindi atachuana dhidi ya mshindi kati ya Paris Saint-Germain au Arsenal.
Flick amethibitisha kuwa kikosi chake cha kusafiri kwa ajili ya mechi hiyo ya marudiano kitakuwa na jumla ya wachezaji 23.
Habari kuu ni kwamba Lewandowski amerudi kwenye kikosi baada ya kukosa mechi nne zilizopita kutokana na majeraha kwenye paja lake la kushoto.
Hata hivyo, Jules Kounde hatakuwepo baada ya kuondolewa uwanjani kipindi cha kwanza katika mechi ya kwanza Jumanne iliyopita.



