Kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni kutoka Defensa Central, nyota mchanga wa Olympiacos, Christos Mouzakitis, yuko kwenye rada ya Los Blancos kama mchezaji anayelengwa kutokana na uwezo wake wa kuongoza mashambulizi kupitia katikati ya uwanja na umahiri wake wa kupiga pasi za umbali tofauti.
Taarifa hiyo inaongeza kuwa Real Madrid wanamwona kama ‘Luka Modric mpya’, na wanatumai kuwa ataweza kujaza pengo aliloacha nyota huyo wa Kroatia baada ya kuondoka msimu uliopita.
Kwa mujibu wa chanzo hicho cha Uhispania, viongozi wa Real Madrid wanafuatilia kwa ukaribu sana maendeleo ya Mouzakitis, lakini hawako peke yao katika mbio za kumwania.
Vilabu kama Benfica, Porto, AC Milan, Manchester United na Arsenal pia vinaonyesha nia ya kumsajili, hivyo kuwa washindani wakuu wa Real Madrid.

Kwa upande wa Olympiacos, hii minong’ono na mvuto mkubwa kutoka vilabu vikubwa imekuwa sababu tosha ya kupandisha thamani ya mchezaji.
Wakati thamani ya Mouzakitis sokoni ikiwa ni €15 milioni, ukweli kwamba vilabu vingi vikubwa vinamuhitaji na mkataba wake wa sasa unaodumu hadi mwaka 2029 umeifanya Olympiacos kudai €40 milioni, na hawatakubali senti moja chini ya kiasi hicho.
Hata hivyo, Real Madrid wanapanga kuwasilisha ofa ya €25 milioni, na bado haijulikani kama kutakuwa na maafikiano.
Mpaka sasa msimu huu, kijana huyo mwenye umri wa miaka 18 tayari ameanza michezo mitano ya ligi na mechi tano za UEFA Champions League na alicheza dakika zote 90 katika ushindi wa Real Madrid wa 4-3 dhidi ya Olympiacos.