Klabu ya Manchester City wamelaani unyanyasaji “mbaya” wa kibaguzi kutoka kwa mashabiki wa Sevilla dhidi ya Rico Lewis wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa siku ya Jumatano, wakisema “hatutavumilia ubaguzi wowote”.

Ilikuwa ni mechi ya kukumbukwa ya Lewis mwenye umri wa miaka 17 kwenye Uwanja wa Etihad baada ya mchezaji huyo kupachika bao la kusawazisha katika dakika ya 52 huku akifanyiwa ubaguzi kutoka kwa mshabiki wa Sevilla.
Taarifa ya klabu ilisema kuwa; “Manchester City inalaani vikali unyanyasaji wa kibaguzi ambao Rico Lewis alifanyiwa kutoka kwa wafuasi wa Sevilla kwenye mechi ya jana, tunaelewa kwamba watu wawili wamekamatwa na wanaendelea kufanya kazi na Sevilla na GMP [Polisi Kuu ya Manchester] kuchunguza suala hili”.

City imesema kuwa haitavumilia ubaguzi wa aina yoyote katika uwanja wao na watakuwa wakitoa usaidizi wao kamili kwa Rico kufuatia matukio hayo mabaya huku klabu ya Sevilla ikisema kuwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa iwapo wahalifu hao wawili watathibitika kuwa na hatia.
Taarifa kutoka Laliga imesema kuwa; “Sevilla inalaani vikali tabia ya mashabiki wawili katika sehemu ya nje ya uwanja wa Manchester City, ambao walitambuliwa na kushutumiwa kwa madai ya kuwa na tabia ya kibaguzi dhidi ya mchezaji wa Manchester City Rico Lewis,”.
Klabu hiyo ya Uhispania sasawanasubiri uthibitisho rasmi wa ukweli kuhusu malalamiko yaliyotolewa na City, na ikiwa itathibitishwa, mashabiki hao wawili wataondolewa kwenye orodha wa wanachama.

Pia Sevilla imeeleza kuwa haijawa na matukio yoyote ya ubaguzi wa rangi au chuki dhidi ya wageni katika uwanja wao na kwamba mashabiki wake daima wamejitolea katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi
Lewis alifunga bao la kusawazisha katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Sevilla na kuwa mchezaji mdogo zaidi katika historia kufunga bao kwenye mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa.

