Imekuwa tofauti na maisha yalivyokuwa awali kwa nyota huyo na raia wa taifa la Ufaransa kutoka kwenye kile kilichokuwa kinampa nafasi kubwa ya kuanza kikosini hapo hadi kufikia hatua ya kukosa kabisa nafasi ya kupata namba ya kuonesha uwezo wake uwanjani msimu huu. Ikiwa ameshuhudiwa mara chache tu kwa nafasi yake katika kikosi hicho.
Na hadi sasa hali ya kuendelea kusalia ama kuondoka klabuni hapo imebakia kuwa kitendawili kilichokosa jibu kutokana na mchezaji huyo kutopewa njia sahihi endapo ataendelea kusalia hapo au atafute kwa kutimkia msimu ujao. Hili limekuwa tatizo kwa wachezaji wengi sana kushindwa kupewa nafasi ya kuamua kuachana na klabu zao pale zinaposhindwa kuonesha ushirikiano kwao.
Baada ya kupata majeraha namba yake kikosini hapo ilionekana kuchukuliwa na kutumiwa vizuri na wachezaji wengine ambao wameonekana kufanya vizuri pia. Ndani ya klabu hiyo kuna fukuto la kwamba nyota huyo huenda akatimkia kati ya United au Arsenal basi mazingira yake yamekuwa magumu zaidi.
Mshindi huyo wa kombe la dunia tangu awe nje kwa miezi mitano kikosini hapo kutokana na majeraha ameshindwa pia kurejea uwanjani hata baada ya kurejea kwenye uzima wake kutokana na ushindani kutoka kwa Clement Lenglet ambaye amekuwa kwenye ubora zaidi na kuonekana amekuwa muhimili zaidi.
Hali inaonekana itazidi kuwa mbaya kama nyota mwingine Matthijs de Ligt ataingia kwenye hesabu za kikosi hicho; jambo hilo litachochea ushindani zaidi na kufanya maisha ya nyota huyo kuwa yenye sintofahamu zaidi. Hivyo ni jambo la busara kwake kuendelea kupambania kilicho sahihi kwake.
Sio kwamba hafurahii kwanini haanzishwi kikosini hapo, hana wasiwasi juu ya hilo lakini anachokiona tatizo mbele yake ni lini sasa atarejea kwenye ubora wake na kama atapata hizo nafasi kama ilivyokuwa awali. Hilo ndilo linapelekea aone kuna haja ya dhati kuangalia pale ambapo nafasi yake inapiganiwa zaidi.
Kama mchezaji hana wasiwasi kwa kiwango chake kwa sababu anajua ni kitu ambacho anacho hivyo atarejea kwenye ubora wake akipewa nafasi hiyo lakini ugumu zaidi ni pale ambapo haifahamiki kama atapata nafasi kikosini hapo. Kwa hiyo basi tatizo bado linabaki chini ya mikono ya matajiri zake hao.
Sababu ni nini?
Kwa taarifa zilivyo ni kwamba wao kama klabu hawakupendezwa na kuhusishwa kwa mchezaji kujiunga na klabu ya Manchester na wakati huo wao kama klabu wakiwa wanashughulikia suala lake la matibabu hivyo jambo hilo ndilo lililochangia kuibua sura tofauti kabisa kikosini hapo.

