Thibaut Courtois amekuwa na wakati mgumu kwa kipindi kifupi ndani ya Madrid kutokana na aina ya matokeo ambayo anayapata na klabu hiyo akisimama kwenye milingoti miwili kusaidia matokeo kwenye klabu yake. Usajili wake ulikuwa gumzo kutokana na nyota huyo kuchukia maisha ya Uingereza na kutaka kuwa karibu na familia yake Hispania.
Uhamisho wake wa €31.5m bado unaonekana kuwa yalikuwa ni maamuzi mazito mno kwa Madrid kutokana na kiwango kinachooneshwa na nyota huyo kwa sasa. Madrid wameruhusu magoli zaidi ya 35 kitu ambacho sio cha kawaida kwa kikosi hicho na wanahitaji angalau kuzuia wasiweze kuwa na idadi kama hiyo ya magoli ya kufungwa.
Hadi sasa amekwisha cheza mechi zaidi ya 25 lakini ameshindwa kuhimili vishindo vya nafasi yake hiyo kwa kuruhusu magoli mengi ndani ya mechi zake. Ameshuhudiwa akipoteza mechi kwa idadi kubwa ya magoli kama ile ya 5-1 dhidi ya Barcelona, 3-0 mbele ya Sevilla na kurejea kwa Zidane kunaweza kumpa wakati mgumu nyota huyo.
Kutokana na falsafa zake mara nyingi anamuamini sana Keylor Navas na anamtumia nyota huyo. Kama hali itaendelea hivyo maana yake mlinda mlango huyo anaandaliwa safari ya kuondoka klabuni hapo kama klabu hiyo itaridhia kusajili mlinda mlango mwingine. Hatari inakuja kwake maana klabu inarusha jicho lake kwa baadhi ya nyota:
David De Gea, wamekuwa wakifukuzia huduma ya nyota huyu kwa kipindi kirefu sana hadi sasa. Nyota huyo pia anazidi kuwachanganya Madrid kwa uwezo wake wakilinganisha na mahitaji ya klabu yao kwa sasa. Kama likitokea itakuwa biashara nzuri kwa Madrid lakini mbaya kwa United wanaoamini katika msaada wa mlinda mlango huyo kwa kiwango kikubwa. Na suala lake la kusita kusaini kandarasi mpya linawatia tumbo joto sana.
Jan Oblak, uwezo wake sio wa msimu huu pekee, ni kwa kipindi kirefu amekuwa akisaidia kikosi chake kufanya vizuri mbele ya michuano mbalimbali ambayo huwa na klabu zenye majina makubwa. Kila mmoja anajua mchango wa mlinda mlango huyo na mchango wake kwenye safu ya ulinzi. Hakika kati ya klabu zenye safu ya ulinzi basi Atletico hawaachwi nyuma; hilo linatokana na mchango mkubwa wa nyota huyo katika nafasi yake. Kama wapo kibiashara hakika itawalazimu kuingia mifukoni kwa gharama kubwa kumnyakua nyota huyo.
Gianluigi Donnaruma, tangu msimu wa 2015/16 akiwa AC Milan alikuwa akihusishwa na kujiunga na Madrid lakini mambo hayakwenda sawa. Urefu wake na unyumbulifu wake unamfanya kuwa na nafasi ya kuzuia hatari nyingi sana ndani ya kikosi hicho. Kitakwimu hajaruhusu magoli mara mbili ya takwimu za Courtois huku akiwa amekwishacheza mechi sita zaidi yake. Jambo hilo la kihistoria bado linawapa ushawishi Madrid waendelee kumfukuzia nyota huyo.


Povel
Gud news