UONGOZI wa Azam Fc umempa majukumu mazito Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Abdihamid Moallin ya kuifikisha timu hiyo katika hatua ya makundi kwenye michuano ya kimataifa.
Azam ni miongoni mwa timu nne ambazo zitaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa kwa msimu ujao ambapo itashiriki michuano ya Shirikisho.

Akizungumza kutoka Misri, Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema “Tunatarajia kuwa na mchezo mmoja wa kimataifa wa kirafiki Tar 14 kutoka nchi jirani kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wetu wa kwanza wa ligi ambao tutacheza Agosti 17 mwaka huu.
“Sisi kazi yetu imeishia hapa, tumefanya usajili sasa ni namna gani ambavyo kocha anaenda kuandaa timu kwa ajili ya kwenda kupambana ni yeye na benchi lake la ufundi.”
“Kama viongozi hatumwingilii huko tunamwacha ili aendelee kuijenga timu ili kupambana lakini nia yetu kama ilivyo kwa misimu mingine ni kugombea ubingwa wa Ligi Kuu, FA, Mapinduzi na kwenye michuano ya kimataifa tufike mbali katika hatua ya makundi na tukisogea zaidi katika hatua ya robo fainali itakuwa ziada.”

