Kinda wa timu ya Barcelona, Gavi ameshinda Tuzo ya mchezaji bora chipukizi hapo jana kwenye tuzo za Ballon d’Or zilizofanyika jijini Ufaransa.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 18 amekuwa mchezaji wa pili mfululizo wa Barcelona kutwaa tuzo hiyo, inayotolewa kwa mchezaji bora wa Dunia chini ya umri wa miaka 21, baada ya kiungo mwenzake Pedri kupata heshima hiyo mwaka jana.
Gavi amekuwa na ubora mkubwa tangu alipoingia kwenye kikosi cha kwanza cha wababe hao wa Catalan na amezawadiwa kwa mafanikio makubwa msimu wa 2021-22. Uchezaji wa kinda huyo pia ulimfanya aitwe kwenye timu ya Taifa ya Uhispania na anatazamiwa kucheza Kombe lake la kwanza la Dunia nchini Qatar mwaka huu.

Kiungo wa Real Madrid Eduardo Camavinga ndiye aliyeshika nafasi ya pili, huku Jamal Musiala wa Bayern Munich akiwa wa tatu mbele ya Jude Bellingham wa Borussia Dortmund na Nuno Mendes wa Paris Saint-Germain.
Gavi alisema: “Ninajaribu na kujitolea bora wakati wote na kujaribu kujituma kwa njia bora.”
Alicheza mechi 34 za LaLiga msimu uliopita, akifunga mara mbili na kutoa pasi sita za mabao huku akiimarisha ubora wake katikati ya uwanja.


