KUTOKANA na kasi aliyoanza nayo kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy akianzia benchi kunauwezekano mkubwa kiungo Clatous Chama akaanza kikosi cha kwanza.
Chama alitimiza majukumu yake kwa umakini dakika 28 alizozitumia dhidi ya Jwaneng Galaxy alipochukua nafasi ya Willy Onana aliyeanza kikosi cha kwanza.Ikumbukwe kwamba huo ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhack Benchikha Desemba 2 ubao uliposoma Jwaneng Galaxy 0-0 Simba.
Huenda akapewa nafasi ya kuanza kwenye mchezo dhidi ya Waarabu wa Morocco, Wydad Casablanca.
Kuingia kwa Chama kwenye mchezo huo kuliongeza kasi eneo la wapinzani huku pasi zake zaidi ya 11 alizotoa akitumia mguu wake wa kulia zikifika kwa wahusika na alipiga shuti moja ambalo liligonga mwamba dakika ya 90.Benchikha aliweka wazi kuwa hatatumia majina makubwa kwenye upangaji wa kikosi cha kutafuta ushindi bali kila mchezaji atakayeonesha kazi kubwa uwanjani atapewa nafasi.
“Kila mchezaji ana nafasi ya kufanya vizuri na kuwa kwenye kikosi cha kwanza hivyo hakuna mwenye nafasi kikosi cha kwanza kila mmoja ananafasi kuanza akionyesha uwezo atapata nafasi,”.