Klabu ya soka ya KMC imelazimisha sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa NBC uliopigwa katika dimba la Manungu Mkoani Morogoro.
Klabu hizo mbili zimekutana leo katika mchezo wa ligi kuu ya NBC uliopogwa mkoano Morogoro katika dimba la Manungu huku kila klabu ikionekana kutafuta alama tatu muhimu, Klabu ya Mtibwa Sugar ndio walifanikiwa kupata bao la kwanza kupitia kwa beki wake wa kulia Kameta Duchu.
Mchezo huo ulienda mapumziko kwa klabu ya Mtibwa Sugar kuongoza kwa bao moja kwa bila, Lakini kipindi cha pili klabu ya KMC ilikuja kwa nguvu kubwa kuhakikisha inasawazisha bao ambalo walitanguliwa, Dakika ya 77 ya mchezo beki Kameta Duchu anafanya madhambi kwenye eneo la hatari na kusababisha mkwaju wa penati ambao unawekwa kimiani na Sadala Lipangile dakika ya 78 na kufanya KMC kusawazisha bao hilo.
Baada ya mchezo huo kuisha kwa matokeo ya goli moja kwa moja klabu ya Mtibwa Sugar wao wameendelea kusalia kwenye nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi kuu ya NBC wakiwa na alama zao 25 kwenye jumla ya michezo 20 ambayo wameicheza mpaka sasa kwenye ligi hiyo.
KMC wao baada ya kupata alama moja leo dhidi ya klabu ya Mtibwa Sugar wao wameendelea kusalia kwenye nafasi tisa kwenye msimamo wa ligi kuu ya NBC wakiwa na alama 23 kwenye michezo 20 ambayo wameweza kucheza kwenye ligi kuu msimu huu.

