IMEFAHAMIKA kuwa, mshambuliaji wa Dalian Pro ya China, Cesar Manzoki raia wa Afrika ya Kati, anatarajiwa kuwasili Tanzania wiki hii kujadiliana na Simba kuona uwezekano wa kujiunga na kikosi hicho.
Manzoki mwenye asili ya DR Congo, ni kati ya washambuliaji wanaotajwa kuwaniwa vikali na timu hiyo, katika kukiimarisha kikosi chao kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.
Tangu dirisha dogo la usajili lifunguliwe Desemba 16, 2022, Simba imekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji Mrundi, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ kutoka Geita Gold.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa chanzo makini kinasema, mshambuliaji huyo atatua nchini na kukutana na viongozi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba akiongozwa na mwenyekiti wake, Salim Abdallah ‘Try Again’ kwa ajili ya majadiliano kuona uwezekano wa kujiunga na timu hiyo.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, Manzoki amekubali kutua nchini kufanya mazungumzo hayo baada ya yeye mwenyewe kuonesha nia ya kuichezea Simba.
Aliongeza kuwa, wakati Manzoki akitarajiwa kutua nchini, Simba imeingia hofu ya kuongezewa masharti mengine mapya kutokana na jeraha alilolipata akiwa katika klabu yake, ambalo litamfanya arejee uwanjani Machi, mwaka huu.
“Ndani ya wiki hii Manzoki atakuwepo hapa, anakuja kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wetu wa Simba tayari kwa kukamilisha dili lake.
“Wakati akitua nchini, Simba inahofia kupewa masharti mapya ya kimkataba kutokana na klabu yake anayoichezea ya Dalian Pro ya China kumpa ofa kubwa mchezaji huyo.”
Akizungumzia usajili, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Tupo katika mazungumzo na wachezaji wengi watakaokuja kukiongezea nguvu kikosi chetu, tutawatambulisha mara baada ya taratibu zote za usajili kukamilika.”