Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Angel Gamondi, amesema anahitaji wachezaji wake muhimu anaowategemea kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu kuwa fiti, hivyo bado anaendelea na mazoezi ya fiziki, huku kiungo mshambuliaji Maxi Nzengeli akionekana kuangaliwa zaidi katika zoezi hilo.
Amesema licha ya kuwa na wachezaji pungufu wengine wakiwa katika majukumu ya timu za Taifa kwa waliokuwepo wataendelea kuongezewa dozi ya mazoezi kulingana na umuhimu wa mashindano yaliyopo mbele yao ikiwamo Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
Kikosi cha Young Africans kinaendelea kujifua na mazoezi katika Uwanja wa Avic Town, Kigamboni na kinatarajia kucheza mechi ya kirafiki wikiendi hii dhidi ya JKU FC ya visiwani Zanzibar, jijini Dar es salaam.
Nzengeli alionekana kufuatiliwa zaidi kwa sababu ni mchezaji tegemeo zaidi aliyebaki, wengine wakiwa kwenye vikosi vya timu zao za taifa zinazoshiriki AFCON nchini Ivory Coast.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Kocha huyo amesema kuna vita nyingine uwanjani ya kusaka ushindi kwenye mashindarno yanayowakabili kwa kuwa ni muhimu kufanya vizuri na kikubwa ni kupata ushindi Uwanjani.
Amesema wachezaji wake wote ni muhimu kuwa fiti, hasa safu ya kiungo na ushambuliaji kwa ajili ya kuwa kwenye kiwango bora ndani ya timu, kuelekea katika mashindano ambayo wanashiriki.
“Kila mchezaji anatambua umuhimu wa kufanya kazi kwa umakini na kutimiza majukumu ambayo yapo na inawezekana kuwa katika ubora kwenye mechi ambazo tunacheza.”
“Tunahitaji kufanya vizuri katika mashindano hayo matatu yaliyopo mbele yetu, kwanza kutetea mataji yetu ya ubingwa wa ligi na ASFC, pamoja na kuvuka kwenye Robo na kwenda Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa, ambayo inawezekana wachezaji wakipambana,” amesema kocha huyo.