LICHA ya kuwepo kwa taarifa kuwa huenda kocha wa Simba Roberto Oliveira (Robertinho) atakalia kuti kavu kutokana na hali ya mambo kwenye kikosi hicho, lakini mambo ni tofauti kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba Salim Abdallah “Try Again“.
Taarifa za kikachelo ambazo zimepatikana ni kwamba, bosi Salim Try Again anamkingia kifua Robertinho na kwamba hakuna lolote ambalo litamtokea kwa sasa.Salim Try Again amesema kwasasa wanachotaka ni kuona timu inapata ushindi na sio kucheza vizuri au kupiga pasi nyingi ndani ya uwanja kama ambavyo mashabiki wanataka, kwa kuwa mara zote malengo ya timu ni kuchukua ubingwa.
“Bosi amesema kwasasa wamemuacha mwalimu afanye kazi yake na wao kama viongozi wanampa nguvu zote ili kuhakikisha wanapata matokeo. Hakuna kupewa mechi wala kukalia kuti kavu,” alisema mtoa taarifa.Aidha, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally yeye amesema: “Mashabiki hao hao wanaohitaji timu icheze vizuri baadae wakikosa ubingwa mwisho wa msimu watalaumu. Viongozi wamempa mamlaka kocha ya kufanya kazi yake na hatuna shida na hilo na timu inawapasua watu kila siku.”