IKIWA zimesalia siku tatu kabla ya Yanga kucheza na Al Merrekh mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Makamu wa Rais wa Yanga Arafat Haji amesema kuwa watawafanya wapinzani wao daraja la kufikia makubwa Caf.
Arafat Haji alisema, mipango ya kuwamaliza Wasudan hao imeshakamilika na sasa wanasubiri ifike Jumamosi ili waweze kukamilisha hesabu za dakika 90 ambazo zitatoa hatma yao kimataifa.Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo Arafat alisema hawataki kuishia kwenye hatua ya makundi pekee, bali wanataka kufika hadi fainali na ili kufanikiwa katika hilo ni laziwa wawafunge na kuwatoa Al-Merrekh.
“Hatua hii tunataka kufika makundi, lakini malengo yetu makubwa sisi kuwa timu ya kwanza Tanzania kucheza hatua za juu za mashindano ya Afrika.
“Tulisema mwaka jana kama tutacheza mashindano haya kwa hatua za juu kabisa tukaenda kucheza fainali na msimu huu dhamira yetu ni hiyo hiyo kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kuvunja mwiko wa kuishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Arafat Haji.Yanga wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na mtaji wa mabao 2-0 waliyopata kwenye mechi ya kwanza iliyochezwa Rwanda.