KIMENUKA! Ndiyo utakavyoweza kusema kwa sasa baada ya Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba kupitisha panga kwa mastaa ili kuingiza maingizo mapya matatu haraka.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu, Simba itoke kufungwa mabao 5-1 na Yanga katika mchezo wa Kariakoo Dabi, uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam.Mara baada ya mchezo huo, shutuma mbalimbali ziliwahusisha baadhi ya wachezaji waidaiwa kucheza chini ya kiwango huku mashabiki wakiwataka mastaa wanaowatuhumu kuachana nao katika usajili wa dirisha dogo litalofungiliwa Januari, mwakani.
Tetesi zinadai kuwa tayari uongozi wa timu hiyo, umempa taarifa kiungo wake mshambuliaji, Mrundi Said Ntibanzokiza ‘Saido’ kutafuta timu nyingine atakayokwenda kuicheze katika dirisha dogo, kutokana na kutokuwepo katika mipango.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka, katika kikao kilichokaa juzi Jumatatu jioni cha viongozi kwa pamoja wamekubaliana kuwapunguza wachezaji wake nyota walioshuka viwango na wenye umri mkubwa ili kupisha damu changa itakayoleta chanagamoto mpya katika timu.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alizungumzia hilo na kusema kuwa: “Ni lazima uongozi tufanye maamuzi magumu, katika usajili wadirisha dogo, na jukumu hilo tunamuachia kocha wetu mpya atakayekuja kuifundisha timu yetu, kama uongozi tunaamini kabla ya dirisha kufunguliwa kocha atapata nafasi ya kukiangalia kikosi chetu, baada ya hapo tutakaribisha ripoti yake ya usajili.”