LIGI Kuu ya Wanawake Bara (Simba Queens, Yanga Princess) itaendelea tena kesho Jumatano kwa michezo mitano kuchezwa kwenye viwanja vitano tofauti.
Simba Queens ambao walipoteza mchezo wao wa kwanza mbele ya JKT Queens watakuwa kwenye dimba la Black Rhyno Karatu kucheza na The Tigers Queens.
Huku watani wao watashuka kwenye dimba la Uhuru kucheza na Mkwawa Queens, wakijaribu kusaka alama tatu za kwanza msimu huu baada ya kipigo kutoka kwa Fountain Gate Princess.
Kwa upande wa Fountain Gate wao watakuwa kwenye Jimbo la Mtama kule Mkoa wa Lindi wakicheza na Aman Queens kwenye dimba la Nyangao.
Michezo mingine ni kati ya Baobab Queens watakaokuwa kwenye uwanja wa Jamhuri kucheza na Ceasia Queens, wakati JKT Queens watakuwa na kwenye uwanja wa Nyamagana kucheza na Alliance Girls.
Yanga itaongozwa na kocha mpya Sebastian Nkoma, ambaye aliwahi kuiongoza Simba Queens kuipa ubingwa wa ligi kuu msimu uliopita na kuwapa taji la Cecafa.
Nkoma amejiunga na Yanga akitokea The Tigers Queens ambayo ameiongoza kwa mchezo mmoja wa ligi kuu.