Klabu ya Liverpool ambayo inaongozwa na Jurgen Klopp inaripotiwa kuwa kumtaka Ibrahim Sangare kama jibu la udhaifu wao katika safu yao ya kiungo. Ambapo watalazimika kumenyana na wapinzani wao Manchester United kuwania saini ya nyota huyo wa PSV Eindhoven.
United walikuwa wakihusishwa sana na mchezaji huyu majira ya joto, wakati AC Milan, Leicester na Westham pia wakimtaka kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 ambaye alitarajia kuhama kwenye dirisha hili kubwa la usajili lakini alitia saini mkataba wa miaka mitano kuendelea kuwa PSV.
Hata hivyo hilo bado halikuwa ni pingamizi kwa vilabu vinavyojaribu kumtaka kiungo huyo wa timu ya Taifa ya Ivory Coast. Sangare amejidhihirisha kuwa ni kiungo mkabaji wa kiwango cha juu nchini Uholanzi, akiichezea PSV mechi 98 katika misimu miwili iliyopita toka awasili kutoka Toulouse ya Ufaransa.
Liverpool walilazimika kwenda kumsajili kwa mkopo Arthur Melo kutoka Juventus siku ya mwisho wa dirisha la usajili baada ya wachezaji wake wanaocheza kwenye eneo la kiungo kupata majeraha. Lakini watakuwa na hamu ya kupata huduma ya mchezaji huyu Januari ili waweze kuimarisha kikosi chao.